top of page

FURSA ZA UWEKEZAJI NA MUUNGANIKO WA SGR NA UCHUMI WA BULUU, BIASHARA NA UTALII ZAJADILIWA ZANZIBAR

Zanzibar | 30 Julai 2026

East Africa Business Consortium (EABC) kwa kushirikiana na Tanzania National Chamber of Commerce (TNCC), Zanzibar National Chamber of Commerce (ZNCC), Tanzania Railways Corporation (TRC) na Geo Green International wamefanikiwa kuandaa Mkutano wa Fursa za Uwekezaji na Muunganiko wa Reli ya Kisasa (SGR) katika Uchumi wa Buluu, Biashara na Utalii, ukiwa na kaulimbiu:

"Driving Economic Growth Through SGR: Unlocking Blue Economy, Trade, Tourism and Investment Opportunities."

Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa sekta ya umma na binafsi, wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo, wataalamu pamoja na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kujadili namna ambavyo Reli ya Kisasa (SGR) inaweza kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi, biashara na uwekezaji.

Katika majadiliano hayo, washiriki walisisitiza kuwa SGR ni zaidi ya miundombinu ya usafiri; ni nyenzo muhimu ya kuunganisha masoko, kuongeza ushindani wa biashara, kupunguza gharama za usafirishaji wa watu na mizigo, kurahisisha upatikanaji wa masoko mapya na kuimarisha minyororo ya thamani katika sekta mbalimbali za uchumi.

Mkutano ulitoa nafasi ya kujadili fursa zinazotokana na muunganiko wa SGR na sekta za Uchumi wa Buluu, Biashara, Utalii, Uwekezaji, Usafirishaji na Ugavi (Logistics), Uvuvi, pamoja na Utalii na Ukarimu. . Washiriki walieleza kuwa matumizi bora ya SGR yataongeza ufanisi wa biashara za ndani na kikanda, kuvutia uwekezaji mpya na kuongeza ushindani wa Tanzania ndani ya soko la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Majadiliano pia yalionesha umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya sekta binafsi, serikali, taasisi za fedha na washirika wa maendeleo ili kuhakikisha miundombinu ya kisasa inatumika kikamilifu katika kuchochea maendeleo ya uchumi. Washiriki walibadilishana uzoefu na mapendekezo kuhusu namna ya kutumia fursa zilizopo katika kuongeza thamani ya bidhaa, kuimarisha biashara ya kikanda na kufungua masoko mapya kupitia Bandari ya Dar es Salaam pamoja na mtandao wa Reli ya Kisasa (SGR).

Aidha, mkutano uliwezesha kujengwa kwa mitandao mipya ya kibiashara na uwekezaji, ambapo wafanyabiashara, wawekezaji, taasisi za fedha na wadau wengine walipata nafasi ya kuanzisha majadiliano ya ushirikiano yatakayosaidia kutekeleza miradi yenye tija katika sekta mbalimbali za uchumi. Kwa upande wa Zanzibar, mkutano uliangazia pia nafasi ya Uchumi wa Buluu kama moja ya maeneo yenye fursa kubwa za uwekezaji, hususan katika uvuvi, utalii wa bahari, usafirishaji wa majini, huduma za bandari na shughuli nyingine zinazochangia ukuaji endelevu wa uchumi. Hili linaendana na jitihada zinazoendelea za Zanzibar za kuifanya sekta ya Uchumi wa Buluu kuwa moja ya nguzo kuu za maendeleo na uwekezaji.

Kupitia mkutano huu, EABC iliendelea kutekeleza dhamira yake ya kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda kwa kuwaleta pamoja wadau mbalimbali ili kujadili fursa zinazotokana na miundombinu ya kisasa na namna inavyoweza kuchochea maendeleo ya sekta binafsi.

Mkutano umeacha msingi imara wa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma na binafsi, kuhamasisha uwekezaji wenye tija na kuibua mikakati itakayowezesha matumizi bora ya Reli ya Kisasa (SGR) katika kukuza biashara, utalii, uchumi wa buluu na maendeleo ya uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

EABC NA TNCC WAANDAA MJADALA WA KITAIFA WA BIASHARA NA UWEKEZAJI 2026 KUIMARISHA MAGEUZI YA KIDIJITALI KATIKA UWEZESHAJI WA BIASHARA

Dar es Salaam, Tanzania | 30 Juni 2026

East Africa Business Consortium (EABC) kwa kushirikiana na Tanzania National Chamber of Commerce (TNCC) wamefanikiwa kuandaa Annual Trade and Investment Dialogue 2026, kongamano la ngazi ya juu lililofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, likiwa na kaulimbiu isemayo:

"Advancing Trade Facilitation Through Digital Transformation and System Integration."

Mgeni Rasmi katika kongamano hilo alikuwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye aliongoza mjadala kuhusu nafasi ya mageuzi ya kidijitali katika kuimarisha mazingira ya biashara, uwekezaji na ushindani wa uchumi wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Akihutubia washiriki, Mheshimiwa Dkt. Nchemba alisisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia mageuzi ya sera, sheria, kanuni na mifumo ya utoaji huduma. Alieleza kuwa Serikali inaendelea kujenga mazingira rafiki yanayowezesha sekta binafsi kukua, kuvutia uwekezaji na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Aidha, alieleza kuwa matumizi ya teknolojia za kidijitali na ujumuishaji wa mifumo ya taasisi mbalimbali za Serikali ni nyenzo muhimu katika kurahisisha biashara, kupunguza urasimu, kuongeza uwazi na ufanisi wa utoaji huduma kwa wafanyabiashara na wawekezaji. Alibainisha kuwa hatua hizo zitachangia kupunguza gharama za kufanya biashara, kuongeza ushindani wa Tanzania na kuimarisha ushiriki wa nchi katika biashara ya kikanda na Bara la Afrika kupitia AfCFTA.

Kongamano hilo liliwakutanisha viongozi wa Serikali, wadau wa sekta binafsi, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo, pamoja na wataalamu wa biashara na uwekezaji kwa lengo la kujadili fursa na mikakati ya kuharakisha mageuzi ya kidijitali katika kuwezesha biashara na uwekezaji nchini.

Washiriki walijadili umuhimu wa kuunganisha mifumo ya taasisi mbalimbali, kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, pamoja na kutumia teknolojia kama chachu ya kuongeza ufanisi wa utoaji huduma, kurahisisha biashara za mipakani na kukuza biashara ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na masoko ya Afrika kwa ujumla.

Kwa upande wao, EABC na TNCC walisisitiza umuhimu wa kuendeleza majukwaa ya majadiliano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kupata suluhisho endelevu la changamoto zinazoikabili biashara na uwekezaji. Taasisi hizo zilieleza kuwa ushirikiano huo utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza biashara, kuvutia uwekezaji, kuongeza ushindani wa biashara za Afrika Mashariki na kuharakisha maendeleo ya uchumi jumuishi.

Kongamano la Annual Trade and Investment Dialogue 2026 lilihitimishwa kwa mwito kwa wadau wote kuendelea kushirikiana katika kuharakisha mageuzi ya kidijitali, kuunganisha mifumo ya utoaji huduma na kujenga mazingira wezeshi yatakayorahisisha biashara, kuongeza uwekezaji na kuimarisha ukuaji endelevu wa uchumi wa Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.

BUSINESS BREAKFAST MEETING: KUFUNGUA FURSA ZA TANZANIA: UWEKEZAJI KATIKA UTALII, UPATIKANAJI WA MITAJI YA MUDA MREFU NA UJENZI WA MITANDAO YA KIBIASHARA

Arusha, Tanzania | 20 January 2026

East Africa Business Consortium (EABC) kwa kushirikiana na Tanzania National Chamber of Commerce (TNCC) wanaendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kupitia programu mbalimbali zinazolenga kukuza ujasiriamali, kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha na kuwawezesha vijana kiuchumi.

Katika kuendeleza ushirikiano kati ya East African Business Council (EABC) na Tanzania National Chamber of Commerce (TNCC), taasisi hizo kwa kushirikiana na Tanzania Investment and Special Economic Zones Authority (TISEZA) ziliandaa Mkutano wa Business Breakfast uliofanyika tarehe 20 Januari 2026 katika Hoteli ya Gran Meliá, Arusha.

Mkutano huo uliwakutanisha wafanyabiashara, viongozi wa sekta binafsi, wanachama wa TNCC, pamoja na wadau wa sekta ya utalii wakiwemo TATO na HAT. Lengo lilikuwa kujadili fursa za biashara na uwekezaji, kuhamasisha uwekezaji wa ndani, kutangaza programu za ujasiriamali kwa vijana, na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Mkutano huo ulitoa jukwaa la wadau kubadilishana uzoefu, kujenga mitandao ya kibiashara na kutambua fursa mpya za biashara na uwekezaji. 

Kwa sasa, TNCC ina wanachama zaidi ya 30,000 na mtandao unaofikia mikoa yote 26 na wilaya 101 nchini Tanzania. Taasisi hiyo inaendelea kuimarisha huduma zake ili kuendana na mabadiliko ya mazingira ya biashara na fursa za uchumi wa kidijitali. 

Kuanzia Januari 2026, EABC kwa kushirikiana na TNCC wanatarajia kuzindua mradi wa kitaifa wa Ujasiriamali kwa Vijana utakaotekelezwa nchini kote. Mradi huo utalenga kutoa huduma za malezi ya biashara (mentorship), mafunzo ya ujasiriamali, ujenzi wa uwezo, kuongeza thamani ya bidhaa na huduma pamoja na elimu ya fedha. Tumefurahishwa kutambua kuwa uhamasishaji wa uwekezaji kwa vijana ni moja ya vipaumbele vya TISEZA, jambo linaloifanya taasisi hiyo kuwa mshirika muhimu katika jitihada za kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana na kuharakisha maendeleo ya ujasiriamali nchini Tanzania.

 

Mfumo wa Wajasiriamali na Vituo vya Malezi ya Biashara

EABC na TNCC pia wanaendelea kuanzisha na kuboresha Mfumo wa Wajasiriamali (Wajasiriamali Portal) wenye lengo la:

  • Kutoa mafunzo ya kujenga uwezo kwa wafanyabiashara.

  • Kuwezesha upatikanaji wa masoko na fursa za biashara.

  • Kusaidia upatikanaji wa mitaji na elimu ya fedha.

  • Kujenga kanzidata ya taifa ya biashara ndogo na za kati (SMEs) kwa ajili ya kurahisisha utoaji wa huduma za maendeleo ya biashara.

Sambamba na hilo, TNCC inaendelea kutekeleza mradi wa kuanzisha Vituo vya Malezi ya Biashara (Incubation Centres) katika mikoa mbalimbali nchini. Baada ya kuanza na awamu ya kwanza katika mikoa sita, mradi huo unaendelea kupanuliwa ili kuwafikia wajasiriamali katika mikoa mingine na kuongeza mchango wa biashara ndogo na za kati katika maendeleo ya uchumi. 

Lengo la vituo hivi ni kuongeza thamani ya bidhaa na huduma, kuimarisha uwezo wa wajasiriamali, kuboresha upatikanaji wa masoko na kuharakisha ukuaji wa viwanda vidogo na vya kati. Mpango huu pia unalenga kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na upatikanaji wa umeme na maendeleo ya shughuli za kuongeza thamani nchini.

Kupitia miradi hii, EABC na TNCC wanaendelea kujenga mazingira bora ya biashara, uwekezaji na ujasiriamali yatakayochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa Watanzania.

BUSINESS BREAKFAST MEETING: KUFUNGUA FURSA ZA TANZANIA KUPITIA UWEKEZAJI, MASOKO, MITAJI YA MUDA MREFU, BIMA NA MAENDELEO YA MAUDHUI YA NDANI

Dar es Salaam, Tanzania | 1 Desemba 2025

Mkutano huo uliokuwa na kauli mbiu “Unlocking Tanzania Potential – Investment Opportunities, Access to Markets, Access to Long-Term Capital, Insurance for Business Growth and Local Content” uliwakutanisha zaidi ya washiriki 300 kutoka sekta mbalimbali za biashara na uwekezaji. Mada iliyowasilishwa na Tanzania Investment and Special Economic Zones Authority (TISEZA) kuhusu fursa za uwekezaji na vivutio vya uwekezaji nchini ilipokelewa kwa hamasa kubwa na kupongezwa na washiriki wa mkutano huo.

East Africa Business Consortium (EABC) na Tanzania National Chamber of Commerce (TNCC) waliandaa Mkutano wa Business Breakfast uliofanyika tarehe 26 Novemba 2025 katika Hoteli ya Serena, ukileta pamoja wafanyabiashara, wanachama wa TNCC, viongozi wa sekta binafsi, TISEZA, TRA pamoja na wadau wengine muhimu wa maendeleo ya biashara na uwekezaji.

Mkutano huo uliandaliwa kwa malengo yafuatayo:

  • Kujadili fursa za biashara na uwekezaji katika kipindi cha muhula wa sita wa Serikali.

  • Kuelimisha wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa bima katika kudhibiti na kupunguza hatari zinazoweza kuathiri biashara, ikiwemo majanga ya moto na hasara nyingine za kiuchumi.

  • Kuweka msingi wa uzinduzi wa Mfumo wa Wajasiriamali (SME Portal) na programu za vituo vya ubunifu na malezi ya biashara (Incubation Programmes) zitakazotolewa kwa njia ya mtandao na ana kwa ana.

Ushirikiano na Sekta ya Bima

Katika juhudi za kuimarisha ustahimilivu wa biashara za ndani, EABC na TNCC zimeendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya bima ili kutoa elimu na uelewa kuhusu usimamizi wa hatari za biashara. Kupitia mikutano ya Business Breakfast iliyofanyika Dar es Salaam tarehe 01 December 2026  washiriki walipata fursa ya kujifunza kuhusu mada ya: “Insurance for Business Growth – Managing Risk and Unlocking Opportunities” Mada hiyo ililenga kuwasaidia wafanyabiashara kuelewa namna bima inavyoweza kuwa nyenzo muhimu ya kulinda biashara dhidi ya hatari mbalimbali na kuwezesha ukuaji endelevu wa biashara.

TAASISI ZA EABC NA UCC ZAFANYA MAZUNGUMZO YA USHIRIKIANO KATIKA KUKUZA UBUNIFU NA UJUZI KWA VIJANA KUPITIA TEKNOLOJIA.

East Africa Business Consortium (EABC) imekutana na University of Dar es Salaam Computing Centre (UCC) kwa mazungumzo yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizi mbili katika eneo la teknolojia. Mazungumzo haya yameangazia njia za kuwawezesha vijana kupitia ubunifu wa teknolojia ili kuwasaidia kujijenga na kujikuza kiuchumi, huku wakiwahamasisha kutoka kwenye fikra za kutegemea ajira pekee na kutazama ujasiriamali kama fursa.

Mazungumzo haya yaliongozwa na Afisa Mtendaji wa EABC, Ndugu Imani Kajula, na Mkurugenzi Mtendaji wa UCC, Ndugu Leticia Ndongole. Wakati wa mazungumzo, viongozi hawa walisisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu kati ya sekta ya biashara na taasisi za elimu ili kuwapatia vijana nyenzo na ujuzi unaohitajika kwa maendeleo yao binafsi na ya nchi.

Afisa Mtendaji wa EABC, Ndugu Kajula, alibainisha kuwa, "Teknolojia ni kichocheo muhimu cha maendeleo, na ni jukumu letu kama wadau kuhakikisha kuwa vijana wanapata maarifa, ujuzi, na mazingira ya kuwa wabunifu na kujenga mustakabali wao." Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa UCC, Leticia Ndongole, alisisitiza kuwa, "UCC inaendelea kuwa chachu ya mabadiliko ya kidigitali kwa vijana kupitia mafunzo na ubunifu wa kiteknolojia. Ushirikiano huu unafungua ukurasa mpya wa fursa kwa vijana. Pia aliishukuru sana EABC kwa kuanzisha mahusiano haya"

Mazungumzo haya ni sehemu ya juhudi za EABC katika kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha miradi yao inayolenga maendeleo ya vijana. EABC na UCC wamekubaliana kuweka mipango madhubuti ya utekelezaji wa miradi hii kwa manufaa ya pande zote mbili na jamii kwa ujumla.

wajasiriamali

EABC YAZINDUA DARASA LA WAJASIRIAMALI

East Africa Business Consortium (EABC) imezindua na kuendesha darasa la kwanza kwa wajasiriamali liitwalo WAJASIRIAMALI DARASA likilenga kuwajengea uwezo wa kuanzisha au kukuza biashara zao kwa njia bunifu na zenye tija. Darasa hili ni moja ya mipango endelevu ya mafunzo ambayo EABC imeanzisha kwa lengo la kuwajengea uwezo. Moja ya njia mahususi kwenye mafunzo haya ni kutumia Wafanya biashara wenye ujuzi na mafanikio ili kuwapa washiriki mafunzo halisi badala ya nadharia.

Darasa hili la kwanza lililoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kapilla Group, Ndugu Gabriel Mwang’onda akiwasilisha mada kuu tatu ambazo ni Wazo na Fursa za Biashara, mada hii ililenga kuwasaidia wajasiriamali kutambua mawazo mapya na jinsi ya kubadilisha changamoto kuwa fursa za biashara.Ubunifu na Uvumbuzi wa Biashara, mada hii ilihimiza wajasiriamali kutumia ubunifu katika kuboresha bidhaa na huduma zao.Uchambuzi wa Masoko na Mahitaji ya Wateja: Mada hii ilitoa mwongozo wa jinsi ya kufanya uchambuzi wa kina wa masoko na kuelewa mahitaji ya wateja kwa ufanisi.

Darasa hili lilihudhuriwa na zaidi ya watu 50, huku likiwafikia watu zaidi ya 16,000 kupitia mitandao ya kijamii na channel ya Youtube EABC Extra Mile. Ushiriki mkubwa huu unaonyesha hamasa na mahitaji makubwa ya mafunzo kama haya miongoni mwa wajasiriamali.      

Kama hukushiriki na utapenda kujifunza basi bonyeza link hii hapa chini ya YouTube channel ya EABC Extramile kwenye link.  https://www.youtube.com/watch?v=ycWj_8dhm1w&t=38s .  Baada kuingia tafadhali follow ili uwe unapata taarifa na mafunzo mengine.

Akimshukuru Mwezeshaji wa darasa hili, Afisa Mtendaji Mkuu wa EABC Imani Kajula alisema ‘’tutaendelea kuwaletea madarasa zaidi yenye lengo la kuwajengea wajasiriamali uwezo wa kukabiliana na changamoto za soko, kukuza biashara zao,kupata mitaji, kuongeza uwezo wao kushindana sokoni na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi’’.

AFISA MTENDAJI MKUU WA EABC AKUTANA NA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU WA KAZI , VIJANA, AJIRA, NA WENYE ULEMEVU MH. RIDHIWANI KIKWETE.

EABC kupitia moja ya nguzo zake kuu ya ushirikishaji wa Serikali, Kampuni binafsi na Taasisi za wanachama imeendelea kushirikisha wadau muhimu katika utekelezaji wa program zake. Wiki hii Afisa Mtendaji Mkuu wa EABC akiwa na Mkuu wa Miradi wa EABC Levina Makwasa walifanya mazungumzo na Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi Ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana , Ajira na Wenye Ulemavu Mh.Ridhiwani Kikwete ofisini kwake.

 

Mazungumzo hayo yalijikita katika kumweleza Mh, Ridhiwani Kikwete juu ya program za EABC na maeneo ambayo yanahitaji ushirikishwaji na ushiriki wa Serikali . Akizungumza wakati wa mkutano huo Afisa Mtendaji Mkuu Imani Kajula alisema ‘’ kama EABC tunaamini kwa dhati kuwa mikakati ya ukuzaji ajira, ujuzi na ujasiriamali ni mikakati inayohitaji ushirikiano kati ya sekta binafsi, asasi na pia serikali ili kuwa na maendeleo jumuishi na yenye tija kubwa’’. Kajula alimaliza kwa kusema tunashukuru sana kwa utayari wa Serikali wa kuwa tayari kushirikiana na sekta binafsi na asasi kama yetu katika kuhakikisha tunakuza ajira, uchumi na kuleta maendeleo jumuishi’’.

 

Kwa upande wake Waziri Mh Ridhiwani Kikwete alisema ‘’ Serikali yetu ipo tayari kushirikiana na EABC katika kuhakikisha vijana wanapata ajira, ujuzi na kuweza kutumia fursa nyingi zilizopo Nchini kwetu. Wizara yetu ipo tayari kushirikiana na EABC katika program zake zenye lengo la kuleta tija na maendeleo jumuishi ya Watanzania hususani vijana ambao ni wengi’’

TAASISI ZA  TNCC  NA EABC ZAINGIA MAKUBALIANO.

Tanzania National Chamber of Commerce (TNCC) na East Africa Business Consortium (EABC) leo tarehe 18 Novemba 2024, wameingia kwenye makubaliano ya ushirikiano (MOU) ili kukuza Ujasiriamali nchini Tanzania hususani kwa vijana.

TNCC ikiwa ni taasisi yenye zaidi miaka 30 Nchini Tanzania inafanya kazi zake kwenye mikoa 26 na wilaya 150 Nchini Tanzania. TNCC imekua mbia mkubwa wa uendelelezaji wa biashara, viwanda na kilimo nchini Tanzania. Kwa upande wake EABC ni taasisi iliyojikita katika kuendeleza Ujasiriamali, Utalii, Ubunifu na miradi ya kukuza ajira kwa vijana.

Mabuliano haya yanalenga kutumia uzoefu wa taasisi hizi mbili kuleta maendeleo makubwa katika kukuza ujasiriamali nchini Tanzania hususani kwa vijana. Takwimu zinaonyesha Zaidi ya asilimia 80% ya Watanzania ni Vijana chini ya miaka 40. Moja ya changamoto kubwa wanazopata vijana ni ukosefu wa ajira, hivyo ushirikiano wa TNCC na EABC unalenga kukuza ujasiriamali kama njia ya kukuza ajira nchini Tanzania. Kupitia makubaliano haya taasisi hizi mbili zitashirikiana katika kuendesha mafunzo na mikakati mingine ya kukuza ujasiriamali nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Afisa Mtendaji Mkuu wa EABC Imani Kajula alisema ‘’ Tanzania ni moja kati ya Nchi 43 zilizokubali kuanzishwa kwa soko huru la Afrika yaani afCFTA ambalo linatoa fursa pana kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa KiTanzania kunufaika na soko hili kubwa, pili ajira kwa vijana ni moja ya changamoto kubwa hivyo mikakati ya kukuza ujasiriamali inalenga kufanya vijana wengi kuwa na ujuzi na kujikita kwenye ujasiriamali hivyo kutumia fursa nyingi zinazotokana na ukuaji wa uchumi na pia soko pana la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Tunalenga kutengeneza kizazi cha vijana wenye kuona ujasiriamali kama njia bora ya kujiajiri na hivyo kutoka kuwa waajiriwa hadi kuwa waajiri’’.

Tanzania ina fursa nyingi sana ambazo zinahitaji jicho la kijasiriamali kuweza kuzitumia, hivyo kuwajengea uwezo wa ujasiriamali vijana utakuza uwezo wao wa kutambua na kutumia vizuri fursa zilizopo na zinazokuja. Kwa kutumia uwezo mkubwa wa uendelezaji biashara ilionao, EABC inalenga kutoa mafunzo na kujenga uwezo kwa vijana wengi Nchini Tanzania. Kupitia ushirikiano huu na taasisi kongwe na yenye mtandao mkubwa wa mikoa 26 na wilaya 150 program zetu zitawafikia na kuwanufaisha vijana wengi na hivyo kuakisi dira ya EABC ya kuwa chachu ya ukuaji wa ujasiriamali, alimalizia Ndugu Kajula.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TNCC Oscar Kissanga alisema ‘’ Moja kati ya malengo mahususi ya kuanzishwa kwa TNCC ni kukuza biashara nchi Tanzania, ili tuweze kukuza biashara basi ukuzaji wa Ujasiriamali ni nyenzo muhimu zana katika kukuza Taifa lenye wajasiamali wanaoweza kutumia fursa zilizopo. Tunafurahi kuwa ushirikiano huu unaenda kuwapa mafunzo, uzoefu na mbinu vijana ambao ni kundi muhimu kwa TNCC. Kupitia mikakati yetu na malengo yetu ya kuwa karibu na vijana TNCC ilianzisha uanachama wa Vijana.

Hivyo ushirikiano huu unaenda kunufaisha vijana wengi Nchini Tanzania. Ni furaha yetu kama TNCC kushirikiana na taasisi zenye malengo makubwa ya kukuza biashara na ujasiriamali Nchini Tanzania’’.

©designed by gofinventures

bottom of page