top of page

TAASISI ZA EABC NA UCC ZAFANYA MAZUNGUMZO YA USHIRIKIANO KATIKA KUKUZA UBUNIFU NA UJUZI KWA VIJANA KUPITIA TEKNOLOJIA.

East Africa Business Consortium (EABC) imekutana na University of Dar es Salaam Computing Centre (UCC) kwa mazungumzo yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizi mbili katika eneo la teknolojia. Mazungumzo haya yameangazia njia za kuwawezesha vijana kupitia ubunifu wa teknolojia ili kuwasaidia kujijenga na kujikuza kiuchumi, huku wakiwahamasisha kutoka kwenye fikra za kutegemea ajira pekee na kutazama ujasiriamali kama fursa.

Mazungumzo haya yaliongozwa na Afisa Mtendaji wa EABC, Ndugu Imani Kajula, na Mkurugenzi Mtendaji wa UCC, Ndugu Leticia Ndongole. Wakati wa mazungumzo, viongozi hawa walisisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu kati ya sekta ya biashara na taasisi za elimu ili kuwapatia vijana nyenzo na ujuzi unaohitajika kwa maendeleo yao binafsi na ya nchi.

Afisa Mtendaji wa EABC, Ndugu Kajula, alibainisha kuwa, "Teknolojia ni kichocheo muhimu cha maendeleo, na ni jukumu letu kama wadau kuhakikisha kuwa vijana wanapata maarifa, ujuzi, na mazingira ya kuwa wabunifu na kujenga mustakabali wao." Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa UCC, Leticia Ndongole, alisisitiza kuwa, "UCC inaendelea kuwa chachu ya mabadiliko ya kidigitali kwa vijana kupitia mafunzo na ubunifu wa kiteknolojia. Ushirikiano huu unafungua ukurasa mpya wa fursa kwa vijana. Pia aliishukuru sana EABC kwa kuanzisha mahusiano haya"

Mazungumzo haya ni sehemu ya juhudi za EABC katika kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuimarisha miradi yao inayolenga maendeleo ya vijana. EABC na UCC wamekubaliana kuweka mipango madhubuti ya utekelezaji wa miradi hii kwa manufaa ya pande zote mbili na jamii kwa ujumla.

EABC YAZINDUA DARASA LA WAJASIRIAMALI

East Africa Business Consortium (EABC) imezindua na kuendesha darasa la kwanza kwa wajasiriamali liitwalo WAJASIRIAMALI DARASA likilenga kuwajengea uwezo wa kuanzisha au kukuza biashara zao kwa njia bunifu na zenye tija. Darasa hili ni moja ya mipango endelevu ya mafunzo ambayo EABC imeanzisha kwa lengo la kuwajengea uwezo. Moja ya njia mahususi kwenye mafunzo haya ni kutumia Wafanya biashara wenye ujuzi na mafanikio ili kuwapa washiriki mafunzo halisi badala ya nadharia.

Darasa hili la kwanza lililoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kapilla Group,Ndugu Gabriel Mwang’onda akiwasilisha mada kuu tatu ambazo ni Wazo na Fursa za Biashara, mada hii ililenga kuwasaidia wajasiriamali kutambua mawazo mapya na jinsi ya kubadilisha changamoto kuwa fursa za biashara.Ubunifu na Uvumbuzi wa Biashara, mada hii ilihimiza wajasiriamali kutumia ubunifu katika kuboresha bidhaa na huduma zao.Uchambuzi wa Masoko na Mahitaji ya Wateja: Mada hii ilitoa mwongozo wa jinsi ya kufanya uchambuzi wa kina wa masoko na kuelewa mahitaji ya wateja kwa ufanisi.

Darasa hili lilihudhuriwa na zaidi ya watu 50, huku likiwafikia watu zaidi ya 16,000 kupitia mitandao ya kijamii na channel ya Youtube EABC Extra Mile. Ushiriki mkubwa huu unaonyesha hamasa na mahitaji makubwa ya mafunzo kama haya miongoni mwa wajasiriamali.      

Kama hukushiriki na utapenda kujifunza basi bonyeza link hii hapa chini ya YouTube channel ya EABC Extramile kwenye link.  https://www.youtube.com/watch?v=ycWj_8dhm1w&t=38s .  Baada kuingia tafadhali follow ili uwe unapata taarifa na mafunzo mengine.

Akimshukuru Mwezeshaji wa darasa hili, Afisa Mtendaji Mkuu wa EABC Imani Kajula alisema ‘’tutaendelea kuwaletea madarasa zaidi yenye lengo la kuwajengea wajasiriamali uwezo wa kukabiliana na changamoto za soko, kukuza biashara zao,kupata mitaji, kuongeza uwezo wao kushindana sokoni na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi’’.

AFISA MTENDAJI MKUU WA EABC AKUTANA NA WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU WA KAZI , VIJANA, AJIRA, NA WENYE ULEMEVU MH. RIDHIWANI KIKWETE.

EABC kupitia moja ya nguzo zake kuu ya ushirikishaji wa Serikali, Kampuni binafsi na Taasisi za wanachama imeendelea kushirikisha wadau muhimu katika utekelezaji wa program zake. Wiki hii Afisa Mtendaji Mkuu wa EABC akiwa na Mkuu wa Miradi wa EABC Levina Makwasa walifanya mazungumzo na Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi Ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana , Ajira na Wenye Ulemavu Mh.Ridhiwani Kikwete ofisini kwake.

 

Mazungumzo hayo yalijikita katika kumweleza Mh, Ridhiwani Kikwete juu ya program za EABC na maeneo ambayo yanahitaji ushirikishwaji na ushiriki wa Serikali . Akizungumza wakati wa mkutano huo Afisa Mtendaji Mkuu Imani Kajula alisema ‘’ kama EABC tunaamini kwa dhati kuwa mikakati ya ukuzaji ajira, ujuzi na ujasiriamali ni mikakati inayohitaji ushirikiano kati ya sekta binafsi, asasi na pia serikali ili kuwa na maendeleo jumuishi na yenye tija kubwa’’. Kajula alimaliza kwa kusema tunashukuru sana kwa utayari wa Serikali wa kuwa tayari kushirikiana na sekta binafsi na asasi kama yetu katika kuhakikisha tunakuza ajira, uchumi na kuleta maendeleo jumuishi’’.

 

Kwa upande wake Waziri Mh Ridhiwani Kikwete alisema ‘’ Serikali yetu ipo tayari kushirikiana na EABC katika kuhakikisha vijana wanapata ajira, ujuzi na kuweza kutumia fursa nyingi zilizopo Nchini kwetu. Wizara yetu ipo tayari kushirikiana na EABC katika program zake zenye lengo la kuleta tija na maendeleo jumuishi ya Watanzania hususani vijana ambao ni wengi’’

TAASISI ZA  TCCIA  NA EABC ZAINGIA MAKUBALIANO.

 

Tanzania Chamber Of Commerce, Industry and Agriculture ( TCCIA) na East Africa Business Consortium (EABC) leo tarehe 18 Novemba 2024, wameingia kwenye makubaliano ya ushirikiano (MOU) ili kukuza Ujasiriamali nchini Tanzania hususani kwa vijana.

TCCIA ikiwa ni taasisi yenye zaidi miaka 30 Nchini Tanzania inafanya kazi zake kwenye mikoa 26 na wilaya 150 Nchini Tanzania. TCCIA imekua mbia mkubwa wa uendelelezaji wa biashara, viwanda na kilimo nchini Tanzania. Kwa upande wake EABC ni taasisi iliyojikita katika kuendeleza Ujasiriamali, Utalii, Ubunifu na miradi ya kukuza ajira kwa vijana.

Mabuliano haya yanalenga kutumia uzoefu wa taasisi hizi mbili kuleta maendeleo makubwa katika kukuza ujasiriamali nchini Tanzania hususani kwa vijana. Takwimu zinaonyesha Zaidi ya asilimia 80% ya Watanzania ni Vijana chini ya miaka 40. Moja ya changamoto kubwa wanazopata vijana ni ukosefu wa ajira, hivyo ushirikiano wa TCCIA na EABC unalenga kukuza ujasiriamali kama njia ya kukuza ajira nchini Tanzania. Kupitia makubaliano haya taasisi hizi mbili zitashirikiana katika kuendesha mafunzo na mikakati mingine ya kukuza ujasiriamali nchini Tanzania.

 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Afisa Mtendaji Mkuu wa EABC Imani Kajula alisema ‘’ Tanzania ni moja kati ya Nchi 43 zilizokubali kuanzishwa kwa soko huru la Afrika yaani afCFTA ambalo linatoa fursa pana kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa KiTanzania kunufaika na soko hili kubwa, pili ajira kwa vijana ni moja ya changamoto kubwa hivyo mikakati ya kukuza ujasiriamali inalenga kufanya vijana wengi kuwa na ujuzi na kujikita kwenye ujasiriamali hivyo kutumia fursa nyingi zinazotokana na ukuaji wa uchumi na pia soko pana la Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Tunalenga kutengeneza kizazi cha vijana wenye kuona ujasiriamali kama njia bora ya kujiajiri na hivyo kutoka kuwa waajiriwa hadi kuwa waajiri’’.

 

Tanzania ina fursa nyingi sana ambazo zinahitaji jicho la kijasiriamali kuweza kuzitumia, hivyo kuwajengea uwezo wa ujasiriamali vijana utakuza uwezo wao wa kutambua na kutumia vizuri fursa zilizopo na zinazokuja. Kwa kutumia uwezo mkubwa wa uendelezaji biashara ilionao, EABC inalenga kutoa mafunzo na kujenga uwezo kwa vijana wengi Nchini Tanzania. Kupitia ushirikiano huu na taasisi kongwe na yenye mtandao mkubwa wa mikoa 26 na wilaya 150 program zetu zitawafikia na kuwanufaisha vijana wengi na hivyo kuakisi dira ya EABC ya kuwa chachu ya ukuaji wa ujasiriamali, alimalizia Ndugu Kajula.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TCCIA Oscar Kissanga alisema ‘’ Moja kati ya malengo mahususi ya kuanzishwa kwa TCCIA ni kukuza biashara nchi Tanzania, ili tuweze kukuza biashara basi ukuzaji wa Ujasiriamali ni nyenzo muhimu zana katika kukuza Taifa lenye wajasiamali wanaoweza kutumia fursa zilizopo. Tunafurahi kuwa ushirikiano huu unaenda kuwapa mafunzo, uzoefu na mbinu vijana ambao ni kundi muhimu kwa TCCIA. Kupitia mikakati yetu na malengo yetu ya kuwa karibu na vijana TCCIA ilianzisha uanachama wa Vijana

Hivyo ushirikiano huu unaenda kunufaisha vijana wengi Nchini Tanzania. Ni furaha yetu kama TCCIA kushirikiana na taasisi zenye malengo makubwa ya kukuza biashara na ujasiriamali Nchini Tanzania’’.

©designed by gofinventures

bottom of page